WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII KUEPUSHA VIFO VYA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA.
Posted on: December 21st, 2024Na WAF - PWANI
Imeelezwa kuwa kila mhudumu wa afya ngazi ya jamii akitekeleza jukumu la kuiwezesha jamii kufikiwa na matibabu ya msingi mapema, itaisaidia kuepukana na vifo, umaskini na vilema vinavyochangiwa na kuchelewa kupata matibabu.
Hayo yameelezwa na Mshauri wa Rais Masuala ya Afya na Tiba, na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohammed Janabi leo Disemba 20, 2024.
Prof. Janabi amesema hayo wakati wa ziara yake iliyolenga kupata picha halisi ya mafunzo kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs), Kibaha mkoani Pwani katika vyuo vya Umahiri wa Afya na Sayansi Shirikishi.
“Wewe mhudumu wa afya ngazi ya jamii ukiweza kutoa elimu kwenye ngazi ya msingi mgonjwa hatafika Mkapa, JKCI, MOI, Hospitali ya mkoa wala Muhimbili,” amesema Prof. Janabi.
Katika suala la uzazi salama Prof. Janabi amewataka watoa huduma za Afya wa ngazi ya jamii pindi watakapoanza utekelezaji wa majukumu yao kuhakikisha wanatoa elimu na maarifa ya masuala ya afya kama, umuhimu wa mama kujifungulia kituoni.
“Ninyi mnatoa mchango mkubwa sana wa utekelezaji wa Sera yetu ya Taifa ya Afya ambayo moja ya ajenda yake ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto vitokanavyo na uzazi, hivyo uwepo wenu utachochea kufikia lengo la kupunguza zaidi vifo vya akina mama na watoto,” alisema Prof. Janabi.
Prof. Janabi pia ametumia fursa hiyo kuwapa rai wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushiriki kikamilifu katika kuwezesha jamii kuelewa na kunufaika na Bima ya Afya kwa Wote.
Wakati huohuo, Shirika la Apotheker Health Access Initiative limeshiriki kikamilifu kwa pamoja na wataalam hao wanaoshirikiana nao mkoani Pwani na kumuonesha Prof. Janabi mfumo wa Afya-Tek, ambao umeingizwa rasmi kwenye Mfumo Jumuishi wa Ngazi ya Jamii na jinsi mfumo huo unavyosaidia kuboresha huduma za afya ngazi ya jamii.
Kwa upande wake Afisa Mkuu Ubunifu, Mahusiano na Mikakati AfyaTek, Bi. Fatma Mahmoud amesema lengo kuu la Mradi huo ni kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi na kuboresha afya ya vijana balehe kwa kutumia mifumo ya kidijitali.