HATUA ZA SERIKALI DHIDI YA AFUA ZA UKIMWI ZAPONGEZWA
Posted on: February 12th, 2026Na WAF-Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Johannes Lukumay, imeipongeza Serikali kwa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na UKIMWI nchini, ikiwemo kuwekeza fedha katika huduma za kinga, tiba na matunzo kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NASHCOP).
Mhe. Lukumay amesema hayo leo Februari 11, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati wa wasilisho kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa NASHCOP, akieleza kuwa juhudi za Serikali zinaonesha dhamira ya dhati ya kulinda afya ya Watanzania na kupunguza athari za UKIMWI kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Katika wasilisho hilo, Mwenyekiti wa Kamati amesisitiza umuhimu wa mikakati ya kisera ya kuhamisha taratibu za ununuzi wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs) na kuziingiza kwenye bajeti kuu ya Serikali bila kuyumbisha bajeti ya taifa. Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali imeendelea kuimarisha rasilimali za kukabiliana na UKIMWI kupitia kuanzishwa kwa tozo ya mwitikio wa UKIMWI pamoja na kujumuishwa kwa huduma za magonjwa nyemelezi katika kitita cha Bima ya Afya kwa Wote (UHI).
Dkt. Samizi amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitoa jumla ya Shilingi bilioni 142 kwa ajili ya shughuli za mwitikio wa UKIMWI, huku katika mwaka wa fedha 2025/2026 ikitoa jumla ya Shilingi bilioni 48. Ameongeza kuwa matarajio ya makusanyo ya tozo ya mwitikio wa UKIMWI ni kufikia Shilingi bilioni 250 kwa mwaka huu, ambapo hadi sasa Shilingi bilioni 9.6 tayari zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mwitikio huo.
Kuhusu mifumo, Naibu Waziri amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha uzalishaji wa dawa za ARVs ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa teknolojia za kigeni. Aidha, amesema maboresho ya mifumo ya kidijitali ya huduma za afya yanaendelea ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za huduma na kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa na programu za afya.