Wizara Ya Afya

UIMARISHAJI MIFUMO YA AFYA, USHIRIKIANO WA JAMII NGUZO MUHIMU DHIDI YA EBOLA

Posted on: June 25th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Dar Es Salaam

Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Erasto Silyvanus amesema, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola yanahitaji kuimarishwa kwa mifumo ya afya na ushirikiano wa jamii ni hatua madhubuti za kinga ili kudhibiti milipuko inayoweza kujitokeza siku zijazo.

Akizungumza leo Juni 25, 2026 katika mkutano maalum wa kujadili mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Dkt. Erasto amesema uzoefu wa milipuko iliyopita umeonyesha kuwa changamoto kubwa si tu kudhibiti ugonjwa wakati wa mlipuko, bali pia kushughulikia vyanzo vya maambukizi na sababu zinazochochea kuenea kwake katika jamii.

"Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa imeendelea na uimarishaji wa timu za mwitikio wa haraka ikiwa ni pamoja na utoaji wa mafunzo ya kupambana dhidi ya Ebola katika mikoa yote nchini" amesema Dkt. Erasto

Aidha amesisitiza umuhimu wa kujenga imani kati ya wataalamu wa afya na wananchi, akieleza kuwa ushiriki wa jamii katika kutoa taarifa na kushirikiana na mamlaka za afya ni msingi muhimu katika kufanikisha ufuatiliaji wa mawasiliano ya wagonjwa na kudhibiti maambukizi.

Amebainisha kuwa kutokana na mwingiliano wa kimataifa, magonjwa ya mlipuko yanaweza kuvuka mipaka kwa haraka, jambo linalofanya ushirikiano wa kikanda na kimataifa pamoja na kubadilishana taarifa kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kudhibiti milipuko.

Kwa upande wa hatua za kinga, amehimiza wananchi kuendelea kuzingatia kanuni za usafi binafsi hususan kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka mazingira yanayoweza kuchochea maambukizi kupitia mgusano wa karibu na majimaji ya mwili wa wagonjwa.

Akizungumzia utayari wa kukabiliana na majanga ya afya, alisema nchi zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mifumo ya afya, maabara, rasilimali watu na mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ili kuhakikisha zinakuwa tayari kukabiliana na milipuko inayoweza kutokea wakati wowote.