Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WHO KUENDELEZA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA DHARURA

Posted on: February 14th, 2026

Na WAF, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) Idara ya Dharula na Maafa, pamoja na wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na binafsi imefanya kikao kazi cha tathmini ya athari za kiafya zitokanazo na majanga ya dharura katika Mkoa wa Dodoma.

Katika kikao hicho, washiriki wamejadili kwa kina athari za kiafya zinazotokana na majanga kama mafuriko, ukame, ajali za barabarani, milipuko ya magonjwa ya mlipuko pamoja na majanga ya moto, huku mjadala ukiwa umejikita katika kuimarisha utayari wa sekta ya afya, uratibu wa wadau, pamoja na umuhimu wa elimu kwa jamii ili kupunguza athari kabla na baada ya janga kutokea.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho mgeni rasmi ambaye pia ni  Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Charles Mduma amesema kuwa kama ilivyo mikoa mingine, Dodoma pia inakumbwa na athari za kiafya zitokanazo na majanga ya dharura hususan magonjwa ya mlipuko yanayochagizwa na ongezeko la idadi kubwa ya watu.

"Natambua sio matukio yote mliyoyaandaa yamepewa kipaumbele, hivyo nitoe wito kwa wataalam wetu wote kuendelea kujiandaa na kuweka utayari katika eneo hilo" amesema Bw. Mduma.

Ameongeza kuwa, kwa ngazi ya Mkoa wa Dodoma Ofisi yake ndio inayoshughulika na uratibu wa dharura na maafa, hivyo kupitia kikao hicho mkoa umeyachukulia mafunzo hayo kwa uzito mkubwa, kwani utasaidia katika kufanya mapitio ya mipango ya mkoa katika kukabiliana na dharura na kufanya uhakiki wa kifedha kwa kushirikiana na taasisi hizo ili kuweza kutekeleza mpango kazi ulioandaliwa na wataalam hao.

Aidha, amewapongeza Wizara ya Afya, TAMISEMI, WHO na washiriki hao kwa muda wote waliokaa pamoja na kuandaa mpango kazi huo, huku akisisitiza kuimarishwa kwa mafunzo endelevu kwa watoa huduma za dharura na kamati za kukabiliana na majanga.

Akizungumza kwa niaba ya Mratibu-Udhibiti wa Athari na Majanga kutoka Wizara ya Afya, Dkt James Heller amesema kuwa kupitia mpango kazi huo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau, itaandaa kalenda maalum itakayowezesha kutambua nyakati hatarishi zitakazosaidia kuchukua hatua mapema na kuimarisha