KAMATI YA BUNGE YATAKA TMDA IIMARISHE UDHIBITI WA DAWA NA VIFAA TIBA
Posted on: February 13th, 2026Na WAF-Dodoma,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) kuweka mikakati endelevu ya usimamizi na udhibiti wa dawa na vifaa tiba ili kuboresha ufanisi wa huduma kwa Watanzania.
Akizungumza leo Februari 11, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati wa wasilisho kuhusu TMDA, Dkt. Lukumay amesema kuongeza kasi ya ufuatiliaji na udhibiti wa bidhaa feki ni hatua muhimu, akibainisha kuwa bidhaa hizo huchangia kwa kiwango kikubwa kudorota kwa afya ya wananchi.
Aidha ameshauri kuwa na utaratibu wa kutowaweka watendaji katika nafasi moja kwa zaidi ya miaka 10 ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi wa taasisi kwa baadhi ya watendaji pamoja na kuepusha viashiria vinavyoweza kusababisha mgongano wa maslahi.
Aidha, Dkt. Lukumay ameipongeza TMDA kwa kupata hati safi, akisema hatua hiyo inaonesha uwajibikaji mzuri wa kifedha na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria na taratibu. Ameongeza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kwa wadau na watumishi, jambo linalochangia kuimarisha udhibiti wa dawa na vifaa tiba nchini.
Dkt. Lukumay amesema kamati inalenga kuboresha huduma za afya kwa Watanzania na kuchangia kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2050, hususan lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali kupitia TMDA inaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa baada ya kusajiliwa, kutoa leseni na vibali vya biashara ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi, pamoja na kudhibiti uingizaji na utoaji wa bidhaa nje na ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa TMDA pia hudhibiti matangazo ya biashara ya bidhaa zinazodhibitiwa, hufuatilia madhara ya bidhaa (vigilance) na kufuatilia ubora wa bidhaa zilizopo sokoni ili kulinda afya ya umma.
Hata hivyo, Dkt. Samizi amebainisha kuwa changamoto ya uingizaji wa dawa feki inaendelea kutokana na mipaka mirefu ya nchi, hali inayowezesha dawa zisizosaj