MHE. MCHENGERWA ASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA AFYA WA AFRIKA
Posted on: February 13th, 2026Addis Ababa - Ethiopia
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa leo Februari 13, 2026 ameshiriki kufanya mazungumzo ya pamoja ya Mawaziri wa Afya kwa lengo la kutafuta rasilimali fedha ili kuboresha sekta ya afya akiambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Seif Shekalaghe.
Mkutano huo unafanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika unaofanyika kesho na kesho kutwa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anashiriki na amependekezwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Akichangia katika majadiliano kwenye mkutano huo waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omary amefafanua kuwa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na umuhimu ambao Serikali imetoa hususan katika awamu hii.
Amesema Serikali inachukulia suala la afya kama eneo muhimu katika maendeleo ya watu.
Amesema kwa sasa jambo ambalo linatakiwa kufanyika ni matumizi mazuri ya fedha chache zinazopatikana ili kuwekeza katika eneo la afya, ambapo amesema tafiti zinaonyesha takribani asilimia 20 hadi 40 ya fedha za sekta ya afya zinatumika vibaya.
Kuhusu kufikisha asilimia 15 kwenye sekta ya Afya Mhe Waziri Fedha amesema kiasi konachopelekwa kinazingatia mahitaji halisi.