KITITA CHA AFYA YA MAMA NA MTOTO (UZAZI SALAMA) KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI KWA MAMA NA MTOTO MCHANGA
Posted on: February 14th, 2026Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI inaendelea kutekeleza Mradi wa Kitita Jumuishi cha Huduma za Afya ya Mama na Mtoto Mchanga, unaolenga kuwajengea uwezo watoa huduma za afya, kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kwa kuimarisha ubora wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo yamesemwa leo Februari 13, 2026, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Hassan Rugwa wakati akifungua rasmi Mradi wa Kitita Jumuishi cha Huduma za Afya ya Mama na Mtoto Mchanga katika mkoa huo.
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia maeneo makuu mawili, ambayo ni usambazaji wa vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na utoaji wa mafunzo na mafunzo elekezi kazini kwa watoa huduma, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Tayari baadhi ya vifaa tiba vimeshafikishwa katika Hospitali ya Mkoa, na hatua za mwisho zinaendelea ili kuhakikisha vinafika katika hospitali za wilaya na vituo vya afya,” amesema Bw. Rugwa.
Ameongeza kuwa mradi huo utagusa maeneo muhimu manne, ambayo ni huduma za wajawazito kabla ya kujifungua, huduma za wakati wa kujifungua, huduma za watoto wachanga, pamoja na huduma za mama baada ya kujifungua.
Sambamba na hilo, amezielekeza timu za usimamizi katika ngazi zote ikiwemo Timu ya Usimamizi ya Mkoa (RHMT), Timu ya Usimamizi ya Wilaya (CHMT) pamoja na wasimamizi wa vituo vya afya kuhakikisha wanasimamia mradi huo kwa uwajibikaji na utekelezaji wa vitendo, ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Kigoma itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya, TAMISEMI na wadau wote wa maendeleo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya ndani ya kipindi chote cha utekelezaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya ya Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala, amesema kumekuwepo na changamoto katika huduma za uzazi, hivyo utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto hizo, kwani tayari umeonesha mafanikio katika maeneo mengine nchini unapotekelezwa.