VIONGOZI WATAKIWA KUSIMAMIA VYEMA ZOEZI LA MADAKTARI BINGWA
Posted on: November 12th, 2024
Na WAF – MARA
Mkuu wa mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi amewataka viongozi wote watumie fursa ya Madaktari Bingwa mkoani humo kuhakikisha kila mwananchi mwenye changamoto anafika kuwaona wataalamu na kupata huduma za matibabu ya kibingwa.
Kanali Mtambi ameyasema hayo Novemba 11, 2024 wakati akiwapokea Madaktari Bingwa 63 wa Rais Samia watakaotoa huduma za kibingwa kwa siku sita (6) katika hospitali za halmashauri za wilaya za mkoa wa Mara
“Mwezi huu wa kumi na moja napokea awamu ya pili ya Madaktari bingwa, nitoe rai yangu kwenu viongozi kusimamia vyema zoezi hili kwa kuendelea kuwatangazia wananchi wote wenye changamoto za kiafya kujitokeza kupata huduma karibu na makazi yao, ili kupunguza gharama za kusafiri kufuata huduma hizi,” amesema Kanali. Mtambi.
Kanali Mtambi amewataka madaktari kusimamia huduma kwa kuzingatia taratibu na miongozo ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Huduma hizi ilikuwa ni nadra sana kuzipata ngazi ya halmashauri na ililazimika wananchi kuzifuata hospitali kubwa, tunamshukuru Rais Samia kwani ameamua kuwasafirisha madaktari kuwafuata wananchi kwenye hospitali za wilaya na kupunguza safari, hivyo madaktari mnapaswa kufuta na kusimamia miongozo ya Wizara ya Afya ili kukidhi mahitaji,” amesema Kanali Mtambi.
Kwa upande wake Mratibu wa Madaktari Bingwa kutoka Wizara ya Afya Bw. Joachim Masunga amesema maelekezo ya Serikali kupita Wizara ya Afya ni kuwajengea uwezo wataalamu waliopo ngazi ya msingi ili kupata ujuzi na kuendelea kuwahudumia Watanzania mara baada ya madaktari bingwa kuondoka.
“Serikali imewekeza kwenye vifaa tiba, ingawa kuna baadhi ya maeneo vifaa hivyo bado havijaanza kutumika, sasa twende tukavitumie vifaa hivyo na kuwapatia ujuzi wanataaluma waliopo huko hospitalini ili mkiondoka wao waendelee kutoa huduma kwa wananchi.” amesema Bw. Masunga.
Timu ya madaktari bingwa wa Rais Samia imepiga kambi mkoani Mara kwa siku sita (6) kuanzia Novemba 11 hadi 16, 2024 kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa katika maeneo ya magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto na watoto wachanga, magonjwa ya ndani, upasuaji, na huduma za kinywa na meno.