Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UBORA WA HUDUMA ZA KIBINGWA NGAZI YA MSINGI KUEPUSHA IMANI POTOFU

Posted on: November 12th, 2024

Na WAF, SIMIYU.

Upatikanaji wa huduma bora za afya ngazi ya msingi hususani katika maeneo ya pembezoni mwa vijiji na miji, imetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha wananchi kuachana na imani potofu wanapotafuta tiba.

Hayo yamebainishwa Novemba 11, 2024 mkoani Simiyu na Kaimu Katibu Tawala Mkoa huo Bw. Juma Topera wakati akiwapokea Madaktari Bingwa wa Rais Samia watakakaotoa huduma za kibingwa kwenye halmashauri zote za mkoa huo kwa kipindi cha siku sita (6).

“Wananchi wanakuwa na imani na huduma za hospitali pale zinapoleta suluhu za shida zilizowasumbua kwa muda mrefu, kwani baadhi yao huwa na imani potofu za kishirikina na inaposhindikana huamua kwenda hospitali kupimwa na kupatiwa matibabu, hivyo wakishapona huachana na dhana potofu kuwa walikuwa wamerogwa, ” amesema Bw. Topera.

Ameongeza kuwa taaluma wanayoenda kuipandikiza Mabingwa hao kwa wataalamu wanaowakuta vituoni, itawezesha kuimarisha huduma na kusaidia wananchi kuongeza imani katika huduma za afya ya msingi na za hospitali kwa ujumla.

“Tunajua kwamba hii siyo mara ya kwanza, mlishakuja mara nyingi na kila mnapokuja kunakuwa na matokeo chanya, kwani watendaji wetu wanapata taaluma ambayo hawakuwa nayo hivyo kuimarisha ubora wa huduma hususani katika ngazi ya afya ya msingi na kuongeza tija zaidi katika maeneo ya pembezoni,” amesema Bw. Topera.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia kwa kambi ya Mkoa wa Simiyu, Bi. Jackline Ndanshau amesema taarifa hiyo ya wananchi kuzidisha imani kwa huduma za hospitali ni mafanikio kwa Wizara kwani imetimiza malengo ambayo kambi hizo zilikusudiwa tangu kuanza kwake.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Boniface Marwa amesema ana imani kwa wiki moja wataalamu hao watafanya kazi kubwa kwa jamii na kuongeza tija katika huduma za afya ya msingi za halmashauri.