Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUWEKE MAZIRA RAFIKI YA HEDHI SALAMA KWA USTAWI WA JAMII YETU

Posted on: May 22nd, 2024



Na WAF, Dodoma

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka jamii na wadau kuweka mazingira rafiki kwenye suala la hedhi salama ili mwanamke aweze kutimiza majukumu yake bila kikwazo.

Waziri Ummy ametoa wito huo leo Mei 22, 2024 Jijini Dodoma wakati akitoa Tamko kwa Umma kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Hedhi Salama na uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Hedhi Salama.

"Bila Hedhi salama hakuna ustawi, kwanini tuone kinyaaa kuzungumza masuala ya hedhi salama? amehoji Waziri Ummy na kusema, Suala la hedhi salama hatuwezi kulikwepa ni sehemu ya kuendeleza kizazi katika jamii na taifa kwa ujumla," amesisitiza Waziri Ummy.

Amesema inaposemwa hedhi salama maana yake mhusika anapata elimu bila kikwazo, huduma katika mazingira ya vyoo, uwepo wa usiri, uwepo maji, vifaa salama na utupaji salama wa vifaa vilivyo tumika.

Waziri Ummy amesema kila mwezi wanawake bilioni 1.9 wanakuwa katika kipindi cha hedhi kati ya watu bilioni 7 duniani, ambayo ni asilimia 26 wengi wakiwa ni wenye miaka 15-49.

Aidha Tanzania kwa mujibu wa takwimu za watu na makazi zilizotolewa mwaka 2022 na NBS Wanawake Milioni 14.9 wanachangamoto ya hedging salama hususan ni wale walio na umri wa miaka 15-49.

"Idadi hii ni kubwa hatuwezi kudharau mahitaji yao, hatuwezi kukaa kimya huu ni wajibu wetu kupata hedhi salama kuanzia ngazi ya kaya, Taasisi mpaka jamii," ameeleza Waziri Ummy.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa hedhi isiyosalama inaathari kubwa kwa jamii ikiwemo kupata katika njia ya mkojo (UTI).

Waziri Ummy amesema Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ilifanya utafiti ambapo asilimia 17 ya wasichana walishindwa kuhudhuria masomo kutokana na maumivu ya tumbo, kuogopa fedheha endapo wangechafuka na kukosa vifaa salama.

"Ni matumaini yangu leo tunapozindua maadhimisho ya Hedhi salama itakuwa ni chachu kuwekeza kwenye miundombinu na vifaa ili kuwafanya kuhudhuria mashuleni," amesema Waziri Ummy.

Amesema kuna mitazamo hasi ndani jamii hali inayochangia kumnyima mwanamke kuchangia shughuli za maendeleo.

MWISHO