Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUONDOA USUMBUFU, GHARAMA KWA WANANCHI

Posted on: November 12th, 2024

Na WAF, Geita

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Bw. Mohamed Gombati amesema matarajio ya uongozi wa mkoa huo ni kuona kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia inapunguza gharama za matibabu pamoja na kuondoa usumbufu wa matibabu kwa wananchi wa mkoa wa Geita.

Gombati ameyasema hayo leo Novemba 11, 2024 wakati akiwapokea Madaktari Bingwa wa Rais Samia 49 watakaoweka kambi ya siku sita (6) katika hospitali za wilaya za mkoa wa Geita.

“Wananchi wa Mkoa wa Geita walitakiwa kuzifuata huduma za kibingwa Hospitali ya mkoa Geita, Muhimbili au Bugando lakini kwa sasa watazipata katika hospitali zao za wilaya hivyo kupunguza gharama na usumbufu wa kuzifuata huduma hizo mbali na maeneo yao,” amesema Mhe. Gombati

Aidha, amesema kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia itasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wataalamu wa ndani ya mkoa kwa kuwa uwepo wa madaktari utasaidia kuwajengea uwezo

Gombati ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi katika hospitali za halmashauri ili kupata huduma za kimatibabu za Kibingwa.

Akitoa salamu za Wizara ya Afya, Katibu Afya Mwandamizi Bw. Rahim Ngaweje amezitaka timu za usimamizi za halmashauri za mkoa wa geita kutoa hamasa ya kutosha kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kupata huduma za matibabu za kibingwa ambazo ni nadra kuzipata.

Awali akimkaribisha Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Mganga Mkuu wa mkoa huo Dkt. Omari Sukari amesema, mkoa wa Geita una jumla ya vituo 271 vya kutolea huduma za afya na hospitali tisa (9) zikiwemo za Serikali na binafsi, hivyo wananchi wote watapatiwa huduma za afya katika maeneno yao na kuongeza kuwa ni imani yake mara baada ya kambi ya madaktari bingwa kumalizika, wataalamu wa afya walioko katika hospitali za wilaya watakuwa wameboresha hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kwetu kama mkoa wa Geita ni faraja kubwa kupokea Madaktari hao kwa awamu ya tatu sasa na hivi sasa tayari wananchi wako katika hospitali wakiwasubiri kwa hamu kubwa kupatiwa matatibabu na madaktari bingwa hawa, pia tunaahidi kutoa ushirikiano katika kipindi chote mtakachokuwa mkoani Geita ,“ amesema Dkt. Sukari.