Ministry of Health

TANZANIA, AFRICA CDC WAIMARISHA USHIRIKIANO WA KUENDELEZA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII BARANI AFRIKA

Posted on: June 20th, 2026

Na Mwandishi wetu-Addis Ababa, Ethiopia

Tanzania na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza huduma za afya ngazi ya jamii, kupitia majadiliano yaliyolenga kuweka mikakati ya pamoja ya kuharakisha uwekezaji katika huduma za afya ya msingi kama nguzo muhimu ya kufikia Huduma za Afya kwa Wote (UHC) na malengo ya maendeleo ya afya barani Afrika.

Majadiliano hayo yaliwakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Afya Tanzania na Africa CDC, ambapo walijadili namna ya kuimarisha mifumo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW), matumizi ya teknolojia za kidijitali na Akili Mnemba (AI), mafunzo endelevu, usimamizi wa huduma pamoja na kuongeza uwekezaji wa ndani ili kuhakikisha huduma za afya ngazi ya jamii zinakuwa endelevu na zenye tija kwa wananchi.

Akizungumza tarehe 18, Juni,2026 katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Jamii Africa CDC Dkt. Fidele Ngabo Gaga alibainisha kuwa Tanzania imeendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii, sambamba na juhudi za Bara la Afrika za kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo wanayoishi.

Aidha, alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ameendelea kuonesha uongozi madhubuti unaoweka afya ya jamii na huduma za afya msingi katika nafasi ya juu ya ajenda ya maendeleo ya bara la Afrika.

Ushirikiano huo unaunga mkono azma ya Umoja wa Afrika ya kuwa na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii milioni mbili ifikapo mwaka 2030, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuimarisha ustahimilivu wa mifumo ya afya katika nchi za Afrika.

Majadiliano hayo pia yalisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuboresha utoaji wa huduma, kuimarisha ukusanyaji na matumizi ya taarifa za afya, pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.