Ministry of Health

SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO MPYA JUMUISHI WA KITAIFA WA KUDHIBITI UGONJWA WA SIKOSELI

Posted on: June 19th, 2026

Na Zakayo Mosha – WAF, Kigoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua Mwongozo Mpya Jumuishi wa Kitaifa wa Matibabu na Udhibiti wa Ugonjwa wa Sikoseli (National Sickle Cell Disease Management Guidelines), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kupunguza athari za ugonjwa huo na kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya ndani na nje ya nchi.

Mwongozo huo umezinduliwa leo, Juni 19, 2026, mkoani Kigoma na Mkuu wa Mkoa huo, Mheshimiwa Balozi Simon Sirro, akiyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa Sikoseli Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Maweni, Kigoma.

Akiongea mara baada ya uzinduzi huo, Mratibu wa Huduma za Sikoseli, Himofilia na Magonjwa ya Damu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asteria Mpoto, amesema kuwa mwongozo huo utawasaidia wataalamu wa afya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuboresha huduma kwa wagonjwa wa sikoseli nchini.

“Napenda kumshukuru Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, kwa msukumo na usimamizi wake wa karibu ambao umewezesha kufanikishwa kwa mwongozo huu. Leo tunashuhudia jambo ambalo kwa muda mrefu lilionekana kama ndoto likiwa halisi,” amesema Dkt. Mpoto.

Ameeleza kuwa mwongozo huo umejumuisha huduma za uchunguzi wa ugonjwa wa sikoseli kwa watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, pamoja na taratibu za matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.

Aidha, amesema mwongozo huo umeboreshwa kwa kuingiza huduma za upandikizaji wa uroto, ubadilishaji damu kwa wagonjwa wanaohitaji, pamoja na utoaji wa ushauri nasaha kwa wagonjwa na familia zao.

“Hapo awali tulikuwa na mwongozo uliolenga zaidi uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa sikoseli. Hata hivyo, mwongozo huu mpya umeenda mbali zaidi kwa kujumuisha elimu kwa jamii, ushauri nasaha kwa wagonjwa, pamoja na miongozo ya huduma za kibingwa. Hivyo, utakuwa nyenzo muhimu kwa watoa huduma za afya na wagonjwa wa sikoseli,” amesema Dkt. Mpoto