Ministry of Health

AFRIKA YATAKA MAGEUZI YA HARAKA DHIDI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA KUPITIA PEN-PLUS

Posted on: June 23rd, 2026

Na Atley Kuni, WAF- Dar es Salaam


Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amefungua rasmi Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa PEN-Plus Africa 2026, akisisitiza haja ya mageuzi makubwa ya mifumo ya afya barani Afrika ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).


Mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere International Convention Centre na kuwakutanisha viongozi wa afya, wataalamu na washirika wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali.


Akiongea Juni 23, 2026 wakati wa ufunguzi, Waziri Mchengerwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio kubwa la maendeleo barani Afrika, yakihusisha magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya moyo na mengineyo sugu.


"Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza husababisha zaidi ya vifo milioni 43 kila mwaka kote duniani, sawa na takriban asilimia 74 ya vifo vyote, huku mamilioni wakifariki kabla ya kufikisha umri wa miaka 70", amesema Mchengerwa.


Amesema hali hiyo inaonyesha ukubwa wa changamoto inayokabili mfumo wa afya duniani na Afrika kwa ujumla.


Waziri huyo amesema Afrika imekuwa ikibeba mzigo mkubwa zaidi wa vifo vya mapema kutokana na NCDs, jambo linaloonesha kuwa tatizo hilo si la kiafya pekee bali pia ni la kiuchumi na kijamii.


Akizungumzia hali ya Tanzania, Waziri Mchengerwa amesema vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vimeongezeka kutoka chini ya asilimia 25 miaka ya 1980 hadi asilimia 39 mwaka 2021, huku magonjwa ya moyo yakipanda hadi takriban asilimia 20 ya wananchi.


Waziri Mchengerwa amesema saratani peke yake husababisha takriban vifo elfu arobaini na tano (45,000) kwa mwaka nchini lakini pia magonjwa hayo yamekuwa yakileta mzigo mkubwa wa kiuchumi kwa familia na serikali, ambapo matibabu ya saratani na huduma za kusafisha damu (dialysis) huchukua takriban asilimia 20 ya malipo ya bima ya afya kupitia National Health Insurance Fund (NHIF).