Ministry of Health

KIGOMA YACHUKUA TAHADHARI KUKABILIANA NA MILIPUKO YA MAGONJWA

Posted on: July 21st, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Kigoma

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Damas Kayera amesema mkoa huo umechukua tahadhari mbalimbali za kujiandaa kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Ebola na magonjwa mengine yanayofanana.

Dkt. Kayera amesema hayo leo, Julai 21, 2026, katika mahojiano maalum na wataalamu wa Wizara ya Afya wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini, wazee wa mila, waandishi wa habari na watu mashuhuri katika jamii, wakati wa mafunzo maalum yaliyoandaliwa baina ya Serikali na CIHEB Tanzania

Amesema kutokana na jiografia ya Kigoma kuwa ni miongoni mwa mikoa inayopakana na nchi jirani, Serikali ya mkoa ilianza kuchukua hatua za tahadhari mara baada ya kupokea taarifa za tishio la mlipuko wa Ebola katika nchi jirani.

"Mkoa wa Kigoma ukiwa ni miongoni mwa mikoa ya mipakani, tayari tumechukua tahadhari muhimu tangu tulipopata taarifa za tishio la Ebola katika nchi jirani. Watumishi wote wa afya kuanzia ngazi ya msingi, vituo vya afya hadi Hospitali wamepewa mafunzo na elimu ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo," amesema Dkt. Kayera.

Aidha, amesema mkoa umeimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Idara ya Uhamiaji, ambazo zinafanya kazi katika maeneo yote ya mipaka ya kuingia na kutoka nchini ili kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza.

Dkt. Kayera amesema wataalamu wa afya waliopo katika maeneo ya mipakani wamewezeshwa vifaa maalumu vya uchunguzi kwa wasafiri wanaoingia nchini, ambapo mtu yeyote atakayebainika kuwa na dalili za ugonjwa huo huwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa mujibu wa miongozo ya afya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Kigoma, Abedi Michael, amesema hadi sasa zaidi ya wataalamu 300 wa afya kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Ameongeza kuwa, mbali na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, mkoa umefanikiwa pia kutoa mafunzo kwa zaidi ya wahudumu 280 wa afya ngazi ya jamii pamoja na kusambaza mabango na vipeperushi vyenye ujumbe wa kuelimisha wananchi