WHO, YATAKA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA KIAFYA
Posted on: September 9th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Arusha
Afrika imetakiwa kuongeza uwekezaji wa huduma za afya ya msingi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma sahihi, mahali sahihi na kwa wakati sahihi, kabla hali zao za kiafya hazijafikia hatua ya kuhatarisha maisha.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shilirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Kanda ya Afrika Prof. Mohamed Yakub Janabi wakati wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (PHC), 2026, ulioanza leo Septemba 9, 2026 jijini humo.
Amesema uzoefu wake wa kuwahudumia wagonjwa wenye hali mbaya umeendelea kumfanya kujiuliza iwapo wagonjwa hao wangepata huduma mapema kwenye vituo vya afya vilivyo karibu na maeneo wanayoishi, huenda baadhi yao wasingefikia hatua ya kuwa na hali dhoofu.
Dkt. Janabi ameeleza kuwa huduma za afya ya msingi si suala la kuwa na zahanati pekee, bali ni mfumo unaohakikisha huduma sahihi zinapatikana kwa wakati na karibu na wananchi huku akisisitiza kuwa mifumo imara ya afya ya msingi ina nafasi kubwa ya kugundua magonjwa mapema, kuzuia milipuko, kuendelea kutoa huduma muhimu wakati wa majanga na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na changamoto za kiafya.
Katika hatua nyingine Dkt. Janabi amesema, changamoto za kupungua kwa ufadhili wa afya na athari za janga la COVID-19 zimeonesha umuhimu wa kuwa na mifumo ya afya yenye uwezo wa kustahimili misukosuko.
Ameongeza kuwa nchi zenye mifumo imara na inayobadilika ya huduma za afya ya msingi ziliweza kuendelea kutoa huduma muhimu hata katika vipindi vya majanga.