PROF. JANABI ASISITIZA MPANGO WA PEN-PLUS KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA AFRIKA
Posted on: June 23rd, 2026Na Atley Kuni, WAF-Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika Prof. Mohamed Janabi amesema mpango wa PEN-PLUS kama mkakati muhimu wa kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika.
Prof. Janabi amebainisha kuwa hatua hiyo ni msingi wa kuokoa maisha na kupunguza mzigo mkubwa unaoikabili sekta ya afya katika nchi zinazoendelea.
Akiongea Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kimataifa wa PEN-PLUS unaorushwa kupitia TBC1, Prof. Janabi amesema magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, figo na saratani yamekuwa changamoto kubwa ya kiafya barani Afrika, na hivyo yanahitaji mkakati madhubuti unaowalenga wananchi katika ngazi ya huduma za msingi.
"Mpango wa PEN-PLUS unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa kuzipeleka karibu zaidi na wananchi kupitia hospitali za wilaya na vituo vya afya, badala ya wagonjwa kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu katika hospitali kubwa za rufaa", amesema Prof. Janabi.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kupata matibabu pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya.
Prof. Janabi ameongeza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea pia kuimarishwa kwa uchunguzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, kuongezeka kwa mafunzo kwa wahudumu wa afya, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika ngazi zote za mfumo wa afya.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya ili kupunguza utegemezi wa misaada ya nje, akieleza kuwa mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza unaendelea kukua na unahitaji suluhisho endelevu linalotokana na rasilimali za ndani.
Prof. Janabi amesema iwapo mpango wa PEN-PLUS utatekelezwa kikamilifu, utakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha huduma bora za afya kwa wote (Universal Health Coverage) na kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika.