Ministry of Health

SERIKALI YAWEKEZA ZAIDI BIL.25 KWENYE MIRADI MIWILI OCEAN ROAD

Posted on: June 20th, 2026

Na Clement Robert, WAF – Dar es Salaam

Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 25 katika ujenzi wa jengo la PET-CT Scan la ‘Samia Suluhu Hassan PET Centre’ pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) hatua inayolenga kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini.

Hayo yamebainishwa leo Juni 20, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa uzinduzi wa jengo hilo ambapo amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za afya na kuwasogezea wananchi teknolojia za kisasa za matibabu.

Amesema pamoja na mradi huo, Serikali imeendelea kuwekeza katika mashine mbalimbali za kisasa za matibabu ya saratani zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ikiwemo baadhi ya vifaa vilivyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 18.5, ili kuongeza uwezo wa utoaji huduma kwa wagonjwa nchini.

Mhe. Mchengerwa amewapongeza wataalamu wa afya wa ORCI kwa uzalendo na kujituma kwao, akieleza kuwa tathmini mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na maoni kutoka kwa wagonjwa yameendelea kuthibitisha ubora wa huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo.

“Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia uwekezaji katika miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje ya Tanzania kutafuta matibabu maalumu” amesema Mhe. Mchengerwa

Aidha, amesema mafanikio ya ORCI yanatokana na moyo wa kujitolea wa watumishi wake ambao wameendelea kutoa huduma kwa viwango vya juu, huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuona taaluma yao kama wito wa kuhudumia jamii.