Ministry of Health

PEN-PLUS YAENDELEA KUSOGEZA HUDUMA ZA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA KARIBU NA WANANCHI

Posted on: June 23rd, 2026

Na Mvuda Jaffer, WAF- Dar-es-salaam

Waziri wa Afya amesema mkakati wa PEN-Plus umeendelea kuwa suluhisho muhimu la Afrika katika kuimarisha huduma za magonjwa yasiyoambukiza makali kwa kusogeza huduma hizo karibu na wananchi, hususan katika hospitali za wilaya na vituo vya afya vilivyochaguliwa.

Amezungumza hayo leo Juni 23,2026 Jijini Dar es salaam Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026)

Mhe.Mchengerwa amesema kupitia mpango huo, nchi mbalimbali za Afrika zimefanikiwa kupanua huduma za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa magonjwa yasiyoambukiza makali, hatua inayowawezesha wagonjwa kupata huduma bora bila kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za rufaa za mikoa au taifa.

“Kwa upande wa Tanzania, Serikali imefanya mapitio ya Miongozo ya Matibabu ya Taifa na Orodha ya Dawa Muhimu ili kusaidia utoaji wa huduma maalumu za kitabibu katika ngazi ya huduma za afya ya msingi, ikiwemo tiba ya ndani, huduma za dharura, upasuaji wa kawaida, huduma za uzazi na magonjwa ya wanawake pamoja na huduma za watoto.”amesema Mhe.Mchengerwa

Mhe.Mchengerwa pia ameeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo na Mpango wa Samia Suluhu Hassan Outreach, huduma za PEN-Plus zinaendelea kupanuliwa nchini kote, hususan katika maeneo ya vijijini na maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya.

Mhe.Mchengerwa amesema hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha usawa wa upatikanaji wa huduma, kupunguza gharama kwa wagonjwa na familia zao, pamoja na kupunguza vifo vya mapema vinavyoweza kuzuilika kutokana na magonjwa yasiyoambukiza.