WIZARA YA AFYA YATATHMINI UTAYARI WA HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA MBEYA KUKABILIANA NA EBOLA
Posted on: October 28th, 2026Na Happyness Hans, WAF - Mbeya
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Michael Kiremeji, amesema Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Mbeya kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola kutoka nchi jirani zilizoathiriwa na ugonjwa huo.
Akizungumza leo Oktoba 28, 2026 Jijini Mbeya wakati wa ziara ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dkt. Kiremeji amesema lengo ni kutathmini uwezo wa hospitali hiyo katika kutambua wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola, pamoja na namna ya kuwahudumia kwa usalama.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za awali kwa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na magonjwa ya milipuko, huku hospitali kubwa zenye wataalamu bingwa na bobezi zikitarajiwa kutoa huduma za kibingwa kulingana na mahitaji.
Aidha, Dkt. Kiremeji amesema timu ya Wizara imezungumza na uongozi wa hospitali kuhusu maboresho yanayopaswa kufanyika ili kukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa lengo la kuhakikisha wagonjwa na wahudumu wa afya wanalindwa dhidi ya maambukizi na huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dkt. Prosper Bashaka, ameishukuru Wizara ya Afya kwa ziara hiyo akisema imeongeza fursa ya hospitali kupata mwongozo wa kitaalamu na kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Dkt. Bashaka amesema hospitali imepokea ushauri uliotolewa na timu ya Wizara kwa kushirikiana na timu ya Mkoa wa Mbeya na itaufanyia kazi, ikiwemo kuweka mipango ya muda mrefu itakayosaidia kupunguza maambukizi, maafa na vifo endapo magonjwa ya milipuko yatatokea katika jamii.