WIZARA YA AFYA YAIMARISHA UWEZO WATOA HUDUMA ZA DHARURA KWENYE MAGARI YA WAGONJWA
Posted on: October 13th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kitengo cha Dharura na maafa imeendelea kuimarisha uwezo wa madereva na watoa huduma za afya kwenye magari ya kubebea wagonjwa, kwa kuwapatia mafunzo maalum yanayolenga kuhakikisha wagonjwa wanasafirishwa kwa usalama na kupata huduma stahiki wakati wa dharura.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 13, 2026, na Mratibu wa Huduma za Dharura kutoka Wizara ya Afya, Magdalena Hoya, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wanaohusika moja kwa moja na usafirishaji na utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka.
Bi. Hoya amesema mafunzo hayo yanahusisha madereva wa magari ya wagonjwa pamoja na wataalam wa afya wanaosimamia wagonjwa wakati wa safari, ili kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kutoa huduma zinazofaa na kuimarisha usalama wa wagonjwa kutoka kituo kimoja cha kutolea huduma hadi kingine.
Aidha, amesema kuimarishwa kwa uwezo wa watumishi hao kutasaidia kuongeza ufanisi wa huduma za dharura, hususan katika kuhakikisha wagonjwa wanapata uangalizi na huduma zinazohitajika wakati wa kusafirishwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Taasisi ya Clinton Health Access Initiative (CHAI), Dkt. Leah Mtui, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa madereva na watoa huduma za dharura katika tathmini ya awali ya hali ya mgonjwa, ufuatiliaji wa viashiria muhimu vya uhai.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuimarisha huduma za dharura, hususan kuwajengea uwezo watoa huduma kwenye magari ya wagonjwa, ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma salama, bora na kwa wakati wanapohitaji msaada wa dharura.