WIZARA YA AFYA YAIMARISHA MIKAKATI YA URUTUBISHAJI WA VYAKULA NCHINI
Posted on: October 15th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha mikakati ya urutubishaji wa vyakula nchini kwa lengo la kupunguza upungufu wa vitamini na madini muhimu mwilini, hatua inayolenga kuboresha hali ya lishe na afya ya wananchi.
Haya yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Emmanuel Tayari mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI leo, Oktoba 15, 2026, jijini Dodoma, ikieleza hatua mbalimbali kuhusu mpango na mkakati wa kuimarisha lishe nchini pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha urutubishaji wa vyakula.
Aidha, Wizara imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Urutubishaji wa Vyakula wa mwaka 2026 pamoja na mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wake. Hatua hizo zinaambatana na ukaguzi na upimaji wa ubora wa vyakula ili kuhakikisha viwango vinavyotakiwa vinafuatwa na wazalishaji.
Vilevile, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika uzalishaji wa virutubishi na teknolojia za urutubishaji, ikiwemo kampuni ya SANKU Tanzania Limited inayozalisha mchanganyiko wa virutubishi nchini. Hatua hizo zinaenda sambamba na kuimarisha ufuatiliaji wa ubora na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulaji wa vyakula vyenye virutubishi vya kutosha.