Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAENDELEA KUIMARISHA UWEZO WA WATAALAMU WA AFYA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO WILAYA YA ILEJE

Posted on: July 15th, 2026

Na. Happyness Hans, WAF - Songwe

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ileje, Dkt. Lilian Soteri, amesema ziara ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya katika hospitali hiyo imelenga kufanya ufuatiliaji na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya kuhusu hatua sahihi za kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko wanapotekeleza majukumu yao ya kutoa huduma.

Akizungumza leo Julai 15, 2026, mkoani Songwe. Dkt. Soteri amesema mafunzo hayo yameiwezesha menejimenti pamoja na watumishi wa hospitali hiyo kuongeza uelewa na kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko endapo yatatokea, huku yakichangia kuimarisha usalama wa watoa huduma na wagonjwa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bi. Gloria Valerian, amesema mafunzo yaliyotolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya yameongeza uwezo wa watoa huduma za afya katika hospitali hiyo na halmashauri kwa ujumla wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Bi. Gloria Valerian amesema washiriki wamepata ujuzi wa matumizi sahihi ya vifaa kinga, ikiwemo namna ya kuvaa na kuvua vifaa hivyo kwa usahihi ili kujikinga na maambukizi. Ameongeza kuwa, licha ya baadhi ya magonjwa ya mlipuko kutokuwa yameripotiwa nchini, mafunzo hayo yamewawezesha kuwa tayari kuyakabili endapo yatatokea na yataendelea kuwa msingi wa kuimarisha utoaji wa huduma salama na zenye ubora.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya za kuendelea kuimarisha mfumo wa utayari na mwitikio wa dharura za afya kwa kuwajengea uwezo watumishi wa afya, hatua inayochangia kuimarisha huduma za afya na kulinda afya za wananchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko.