WAZIRI WA AFYA AAGIZA MIKOA KUPIMWA KWA MATOKEO YA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: October 12th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesisitiza uwajibikaji wa viongozi wa mikoa, halmashauri na vituo vya kutolea huduma za afya katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa matokeo yatapimwa kwa kuzingatia huduma zinazotolewa kwa wananchi, upatikanaji wa dawa na matumizi ya bima katika vituo vya afya.
Ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 12, 2026 wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa wote, kilichofanyika jijini Dar es Salaam
Amesema kila kituo kitakuwa na takwimu za hali ya kuanzia na malengo ya utekelezaji kwa kila hatua, huku Mganga Mfawidhi akiwajibika kwa kituo chake, Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Wilaya kwa halmashauri, na Mkuu wa Mkoa kwa matokeo ya mkoa husika.
Aidha, amesema Wizara itatumia mifumo ya kielektroniki kufuatilia malipo na kuhakiki matokeo kwa kulinganisha taarifa za fedha na huduma zilizotolewa, ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unakuwa na tija na unamnufaisha mwananchi.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayenyimwa huduma za afya kwa sababu analipa fedha taslimu au hana kadi ya bima, akieleza kuwa mafanikio ya mpango huo hayatapimwa kwa kupungua kwa malipo ya moja kwa moja pekee, bali kwa kuongezeka kwa wananchi wanaojiunga na kutumia bima zao kupata huduma.
Ameonya kuwa kituo chochote kitakachobainika kumrudisha mwananchi kwa sababu hana bima kitachukuliwa hatua kali, huku akielekeza kuwa kaya maskini zilizotambuliwa zinapaswa kukabidhiwa kadi zao kikamilifu ili ziweze kupata huduma stahiki.
Katika kuimarisha ufuatiliaji, amesema Wizara itatoa taarifa za kila mwezi zinazoonesha hali ya utekelezaji katika mikoa, halmashauri na vituo vya afya kwa kutumia mfumo wa rangi; kijani kwa vituo vilivyofikia malengo, njano kwa vilivyopiga hatua na nyekundu kwa vile ambavyo havijapiga hatua zinazotarajiwa. Taarifa hizo zitawasilishwa kwa viongozi husika na kuwekwa wazi kwa wananchi.