DKT. MAGEMBE: JAMBO UKILIKABIZI KWA WAKUU WA MIKOA HALITAKWAMA
Posted on: October 12th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe ameeleza kuwa ana imani kubwa na ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, wakuu wa mikoa, makatibu tawala na watendaji wa ngazi zote katika kuhakikisha utekelezaji wa jukumu la kuhamasisha bima ya afya kwa wote kwa wananchi unafanyika kwa ufanisi.
Dkt. Magembe ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Kikao Kazi cha Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote
Amesema uzoefu wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya sekta ya afya unaonesha kuwa pale viongozi kama Wakuu wa Mikoa wanapopewa dhamana na kushirikiana kwa karibu, mafanikio yanaweza kupatikana, akitolea mfano wa kupungua kwa vifo vya mama na mtoto pamoja na juhudi za kuboresha hali ya lishe nchini.
Aidha, ameeleza kuwa mafanikio katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya yamewezesha takribani asilimia 85 ya Watanzania kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mbali.
Ameongeza kuwa maandalizi ya utekelezaji wa jukumu hilo yamekamilika na kwamba ni muhimu kuanza kazi huku maboresho madogo yakifanyika kadri utekelezaji unavyoendelea. Amesema kila mkoa utapatiwa taarifa ya tathmini itakayowezesha kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi kwa wakati.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, wakuu wa mikoa, makatibu tawala na watendaji wa ngazi zote ili kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.