KIONGOZI BORA ANAONGOZA KIMKAKATI NA KUANDAA VIONGOZI WA BAADAYE
Posted on: October 11th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesisitiza kuwa kiongozi bora ni yule anayejenga uwezo wa watu anaowaongoza, kuwawezesha kukua kiutendaji na kuandaa viongozi wengine watakaoweza kuendeleza majukumu ya taasisi hata baada ya yeye kuondoka katika nafasi yake.
Dkt. Magembe ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2026 wakati wa muendelezo wa Mafunzo ya Tafakuri (Retreat) ya Viongozi na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Afya yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
"Viongozi wanapaswa kuwapa watumishi nafasi ya kushiriki katika maamuzi, kuwashirikisha katika utekelezaji wa majukumu na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutendaji ili kuongeza ufanisi wa kazi. Kiongozi huwezi kufanikisha malengo ya taasisi peke yako”, amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kuandaa viongozi wa baadaye kwa kuhakikisha maarifa na uzoefu vinaendelezwa ndani ya taasisi, hatua itakayosaidia kudumisha mwendelezo wa utekelezaji wa majukumu na kufikia malengo yaliyowekwa.
Dkt. Magembe amewataka viongozi kuweka mbele maslahi ya taasisi badala ya maslahi binafsi, akibainisha kuwa uongozi wenye tija unahitaji mawasiliano yenye ufanisi, kuaminiana na ushirikiano miongoni mwa watumishi.
Pia, ameeleza kuwa viongozi wanapaswa kuwa tayari kusikiliza maoni ya wengine, kutambua mchango wa watumishi na kutoa mwongozo unaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uwajibikaji.
Akimalizia kuchangia mada ya itifaki iliyotolewa Bw. Omari Kashera, Dkt. Magembe amesisitiza kuwa Mafunzo ya Tafakuri ni fursa muhimu kwa viongozi kutathmini utendaji wao na kuweka mikakati ya maboresho, huku akieleza kuwa mafanikio yake yatapimwa kupitia utekelezaji wa maazimio na kuongezeka kwa ufanisi wa Wizara katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.