Wizara Ya Afya

MHE. MCHENGERWA AWATAKA WAKUU WA MIKOA KUSIMAMIA KIKAMILIFU UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: October 12th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa mujibu wa stahiki zao bila kutozwa gharama ambazo hawapaswi kulipa, akisisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea uongozi thabiti, uwajibikaji na ushirikiano wa ngazi zote za Serikali.

Akizungumza Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Waziri Mchengerwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipa ajenda hiyo kipaumbele kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kukabiliwa na vikwazo vya kifedha vinavyoweza kuathiri maisha yao na familia zao.

Amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 ilipitishwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, akieleza kuwa utekelezaji wake ni sehemu ya dhamana iliyotolewa kwa wananchi na kwamba viongozi wanapaswa kuhakikisha dhamana hiyo inazaa matokeo yanayoonekana katika maisha ya Watanzania.

Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa lengo la mageuzi hayo ni kumwezesha mwananchi kupata huduma anapofika katika kituo cha kutolea huduma za afya, kupokelewa, kupata matibabu na dawa anazostahili kwa mujibu wa mpango husika, bila kudaiwa fedha ambazo hatakiwi kulipa. Amesisitiza kuwa mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote hayatapimwa kwa idadi ya mikutano au maandalizi yaliyofanyika, bali kwa huduma halisi zinazopatikana kwa wananchi.

Katika kusimamia utekelezaji huo, amewataka Wakuu wa Mikoa kuunda na kuongoza wenyewe kamati za mikoa za utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kabla ya uzinduzi, kwa kuwashirikisha Katibu Tawala wa Mkoa, meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, waratibu wa TASAF na wawakilishi wenye mamlaka ya kufanya maamuzi kutoka Bohari ya Dawa (MSD), pamoja na wadau wengine muhimu.