Wizara Ya Afya

WAZIRI WA AFYA ASISITIZA HAKI ZA WANACHAMA WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: October 12th, 2026

Na Clement Robert, WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka watoa huduma za afya kuhakikisha wananchi waliojiunga na Bima ya Afya kwa Wote wanapata huduma wanazostahili kwa mujibu wa vifurushi na masharti ya bima zao bila kunyimwa huduma au kutozwa malipo yasiyoidhinishwa.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2026 wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa wote, kilichofanyika jijini Dar es Salaam

Amesema mwanachama mwenye sifa ya kupata huduma hapaswi kurudishwa bila sababu halali wala kubebeshwa gharama zinazotokana na kituo cha kutolea huduma kushindwa kutimiza wajibu wake. Ameelekeza kuwa dawa inayokosekana katika kituo inapaswa kushughulikiwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kupata suluhisho au huduma mbadala inayofaa.

Aidha, amesisitiza kuwa rufaa zitolewe kwa sababu za kitabibu na kwa maelekezo yanayoeleweka, huku huduma za kuokoa maisha zikitolewa bila kucheleweshwa kutokana na mabishano ya kadi au malipo.

Mhe. Mchengerwa amewataka viongozi kuhakikisha kila kituo kinabandika mahali panapoonekana taarifa za mafao, haki na wajibu wa wanachama pamoja na namba za kupokea malalamiko. Ameeleza kuwa huduma nzuri kwa wananchi ni msingi wa kujenga imani katika mfumo wa bima ya afya.

Katika hatua nyingine, ameelekeza kila halmashauri kuwa na dawati na namba za malalamiko zinazofanya kazi, huku kila malalamiko yakisajiliwa, kupewa kumbukumbu na kufuatiliwa hadi yatakapopatiwa ufumbuzi.

Amesema malalamiko yanayohusu huduma za dharura yanapaswa kushughulikiwa mara moja, huku mengine yakitatuliwa ndani ya siku saba. Malalamiko yanayohitaji maamuzi ya NHIF au Wizara ya Afya yanapaswa kuwasilishwa kwa mamlaka husika bila kuchelewa, na mlalamikaji apewe taarifa kuhusu hatua zilizofikiwa.

Vilevile, amesisitiza kuwa tuhuma za wanachama hewa, madai ya uongo, ada zisizoidhinishwa na matumizi mabaya ya kadi za bima zichunguzwe, na tuhuma zinazohitaji hatua za kisheria zipelekwe kwenye mamlaka husika, ikiwemo TAKUKURU au Jeshi la Polisi, kwa mujibu wa sheria.