MAFUNZO YA TAFAKURI YAIMARISHA UONGOZI WA KIMKAKATI WIZARA YA AFYA
Posted on: October 11th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Mtaalamu wa Itifaki Balozi Omar Kashera Mjenga, amesisitiza umuhimu wa viongozi kuwa na uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi ya kimkakati yanayolenga mafanikio ya muda mrefu, akieleza kuwa uongozi bora unahitaji dira iliyo wazi, uadilifu, nidhamu na utekelezaji wenye tija.
Akizungumza leo Oktoba 11, 2026 Jijini Dar es salaam ikiwa ni siku ya pili ya Mafunzo ya Tafakuri (Retreat) ya Menejimenti ya Wizara ya Afya, Balozi Mjenga amesema uongozi wa kimkakati haupimwi kwa nafasi aliyonayo mtu pekee, bali uwezo wake wa kuelekeza taasisi katika mafanikio yanayotarajiwa.
"Viongozi wanapaswa kujiuliza taasisi ilipo sasa, inataka kufika wapi na mikakati gani itaiwezesha kufikia malengo hayo katika kipindi cha miaka mitano ijayo, mwelekeo ni muhimu kuliko kasi hivyo maamuzi yanapaswa kuzingatia dira ya taasisi na mahitaji ya baadaye," amesema Balozi Mjenga
Akizungumzia upangaji wa mipango, Balozi Mjenga amewataka viongozi kuachana na utaratibu wa kunakili mipango ya awali bila kuchambua mahitaji halisi kwa kuwa mipango ya kimkakati inapaswa kuzingatia ushahidi, takwimu, vipaumbele na matumizi bora ya rasilimali ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Aidha, Balozi Mjenga amesisitiza umuhimu wa viongozi kukabiliana na mabadiliko kwa wakati, kupokea mawazo mapya na kujifunza kutokana na changamoto akibainisha kuwa taasisi zinazoshindwa kubadilika kulingana na mazingira zinaweza kubaki nyuma na kushindwa kufikia malengo yake.
Vilevile, Balozi Mjenga ameeleza kuwa uadilifu na nidhamu ni misingi ya uongozi bora akiwataka viongozi kusimamia maadili, kutenda kwa haki na kuwahudumia watu kwa usawa kwa kuwa tabia za viongozi zina mchango mkubwa katika kujenga imani na utamaduni mzuri wa utendaji kazi ndani ya taasisi.
Pia, Balozi Mjenga amesisitiza umuhimu wa mawasiliano na ushirikiano katika kujenga timu imara, akieleza kuwa kiongozi bora anatofautiana na bosi kwa namna anavyowasikiliza, kuwashirikisha na kuwaongoza wengine katika kufikia malengo ya pamoja.