Wizara Ya Afya

WATUMISHI WA AFYA MARA WAPATIWA MAFUNZO YA UTAYARI WA KUKABILIANA NA EBOLA

Posted on: September 4th, 2026

NA Happyness Hans, WAF - Mara

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dkt. Michael Kiremeji kutoka Wizara ya Afya, amesema watumishi wa afya kutoka halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara wameshiriki mafunzo ya vitendo ya kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola.

Amesema hayo leo Septemba 4, 2026 mkoani Mara amesema mafunzo hayo yanafanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Musoma, ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kutoa huduma endapo kutatokea mgonjwa au mhisiwa wa Ebola.

" kila halmashauri imeshiriki kwa kuleta watumishi wanane, huku mafunzo hayo yakiwa sehemu ya maandalizi yanayofanyika nchini kote, hususan katika mikoa iliyo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa ya milipuko" amesema Dkt. Kiremeji

Aidha Dkt. Kiremeji amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kutoa huduma kwa usahihi na kulinda jamii wakati wa milipuko.

Dkt. Lemens Eliya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), anayeshughulika na masuala ya dharura na maafa, amesema WHO inashirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwawezesha watumishi wa afya kuwa na uelewa sahihi wa namna ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola pia yanalenga kuhakikisha watumishi wanakuwa tayari kuchukua hatua stahiki endapo kutatokea mlipuko, pamoja na kujua namna ya kujikinga wakati wa kutoa huduma, ili kulinda afya zao na ya wananchi.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu, amesema maandalizi ya mapema ni muhimu kwa mkoa huo, kwani yanawapa watumishi uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko endapo yatatokea. Amesema mkoa unashukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha watumishi wa afya wanajengewa uwezo katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Bi. Marieta Kavishe, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Musoma, amesema mafunzo hayo yamewapatia watumishi ujuzi wa kujikinga na maambukizi pamoja na kuwahudumia na kuwatibu kwa usalama wagonjwa na wahisiwa wa magonjwa ya milipuko.