WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW’s) CHACHU YA UTEKELEZAJI MIPANGO YA AFYA NCHINI
Posted on: September 25th, 2024Na. WAF
Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wamekuwa na Mchango mkubwa katika utekelezaji wa Mipango mbalimbali ya Afya ikiwemo Mpango wa Taifa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Malaria, Mpango wa Kudhibiti UKIMWI na Mpango wa Taifa wa Maonjwa Yalisiyopewa Kipaumbele.
Kauli hiyo imebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu ame leo Septemba 24, 2024 Jijini Arusha katika Ufunguzi wa Kikao cha Ushirikiano na Wadau wanaotekeleza Afua mbalimbali za Afya , Lishe na Ustawi wa Jamii kinachoratibiwa na Wizara ya Afya, kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI pamoja na wadau.
Dkt. Machangu amesema kuwepo kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii pamekuwa na mafanikio mengi katika afua za afya.
“Pamekuwa na mafanikio makubwa sana uwepo wa CHW’s, kwenye Programu mbalimbali za HIV, Malaria, Kifua Kikuu na Programu nyinginezo nyingi”, amesema Dkt. Machangu.
Aidha, Dkt. Machangu amesema Mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii yatakayoanza tarehe 30, Septemba, 2024 yatasaidia kwa kiwango kikubwa katika kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika ngazi ya msingi.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Wizara ya Afya Dkt. Norman Jonas amesema Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii utakuwa na mchango mkubwa kusogeza huduma karibu na mwananchi.
Naye Afisa kutoka Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Dkt. Meshack Chinyuli ameongeza kuwa mikoa 10 ya kuanzia inatekeleza mpango huo ili kuhakikisha wananchi wanasogezewa Huduma za afya karibu.
Hata hivyo Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. May Alexander amesema Mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii yatafanyika kwa miezi sita ikiwemo miezi mitatu mafunzo nadharia na miezi mitatu mafunzo kwa vitendo.