Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI RASILIMALI WATU SEKTA YA AFYA MSINGI IMARA MAENDELEO KUELEKEA DIRA 2050

Posted on: July 14th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Uwekezaji wa Rasilimali watu unaofafanuliwa vizuri na Sera ya afya ya mwaka 2007 umetajwa kama msingi wa maendeleo endelevu ya sekta ya afya na nguzo muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, salama na zenye usawa, utu na weledi kuelekea sera ya 2050 sambamba na kufanikisha lengo la huduma za afya kwa wote (UHC).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence leo Julai 14, 2026 wakati akifungua rasmi mkutano wa Nne wa rasilimali watu wa Sekta ya Afya unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam, akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

"Kwa sasa sekta ya afya ina takribani watumishi wa afya laki 182,430 wanaotoa huduma nchini, lakini bado ipo haja ya kuongeza idadi yao na kuhakikisha kunakuwa na msawazo, hususan ni maeneo ya vijijini na maeneo yenye mazingira magumu," amesema Dkt. Samizi

Dkt. Samizi amefafanua kuwa Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii kupitia mpango wa Kitaifa wa uratibu na ujumuishaji wa wahudumu wa Afya ngazi ya jamii, ambapo hadi sasa wahudumu elfu 7,694 wamepata mafunzo, kuajiriwa na kugawanywa maeneo mbalimbali nchini.

"Vilevile, kupitia Samia Health Super-Specialization Program, jumla ya watumishi elfu 2,982 wamefadhiliwa kupata mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa karibu na wananchi ambapo imesaidia kupunguza gharama za kufata huduma hizo nje ya nchi," amesema Dkt. Samizi

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amewataka washiriki wa mkutano huo kutumia majadiliano yao kupata suluhisho la kuandaa nguvu kazi ya afya kwa mahitaji ya baadaye, kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali, kuongeza uwekezaji endelevu na kuwapa vijana nafasi kubwa ya kuleta ubunifu ndani ya sekta ya afya.

Amesisitiza kuwa mageuzi ya rasilimali watu katika sekta ya afya hayawezi kufanikishwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali, taasisi za elimu na utafiti, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kujenga mfumo wa afya wenye nguvu