Wizara Ya Afya

TANZANIA YAWAALIKA WAWEKEZAJI WA MAREKANI KUJENGA KITOVU CHA UZALISHAJI WA BIDHAA ZA AFYA AFRIKA

Posted on: September 3rd, 2026

Na John Mapepele – WAF
Washington, D.C.

Tanzania imewaalika wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, bidhaa za uchunguzi na teknolojia za afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za afya barani Afrika.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, katika Mkutano wa Wadau wa Ushirikiano wa Afya kati ya Marekani na Tanzania uliofanyika Washington, D.C., akisema Tanzania iko tayari kupokea mtaji, teknolojia na utaalamu kutoka kwa wawekezaji wa Marekani.

Mhe. Mchengerwa amesema Serikali inalenga kuibadilisha Tanzania kutoka nchi inayotegemea kwa kiasi kikubwa uagizaji wa dawa na bidhaa za afya kutoka nje na kuwa nchi yenye uwezo wa kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na la kikanda.

Amesema Wizara ya Afya imeanzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (PIAT), kinachowakutanisha taasisi muhimu za Serikali ikiwemo TIC, TMDA, MSD, TRA na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi, kwa lengo la kurahisisha na kuharakisha uwekezaji katika sekta hiyo.

Aidha, amesema Tanzania inaendeleza eneo maalum la kiuchumi kwa ajili ya sekta ya dawa huko Mloganzila, nje ya Dar es Salaam, huku Serikali ikiandaa pia mpango wa Kiwanda cha Taifa cha Uzalishaji wa Chanjo na Bidhaa za Kibiolojia.

Amesema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa kuoanisha mifumo ya kodi na ushuru wa malighafi na vifungashio vya dawa na mifumo ya EAC na SADC, ili uzalishaji wa ndani uwe na ushindani zaidi.

Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania pia imechaguliwa kuwa mwenyeji na kiongozi wa Huduma za Ununuzi wa Pamoja za SADC, hatua inayofungua soko la nchi 16 za SADC kwa wazalishaji watakaoanzisha viwanda nchini.

Amesema fursa hiyo inaifanya Tanzania kuwa eneo lenye mvuto kwa wawekezaji wanaotaka kuzalisha bidhaa za afya kwa ajili ya soko la zaidi ya watu milioni 300 katika ukanda wa SADC, badala ya kulenga soko la Tanzania pekee.