TANZANIA, UINGEREZA WASAINI MKATABA WA NYONGEZA WA HATI YA MAKUBALIANO YA MFUKO WA AFYA WA PAMOJA
Posted on: November 12th, 2024
Na Waf Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Uingereza zimesaini Mkataba wa nyongeza wa Hati ya Makubaliano ya Mfuko wa Afya wa Pamoja wenye lengo la kuimarisha huduma za afya nchini hususan Afya ya Msingi.
Mkataba huo umesainiwa Novemba 12, 2024 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba , Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (OR-TAMISEMI), Dkt. Grace Magembe na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Olukemi Williams ukishuhudiwa na Mwakilishi wa Wadau wa Mfuko wa Pamoja Bi.Franziska Freiburghaus kutoka Uswisi.
Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya nchini ambapo Mwaka 1999, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo walianzisha Mfuko wa Afya wa Pamoja, ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya msingi. Fedha hizo zimekuwa zikitumika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi katika ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
“Tunawashukuru sana wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuitikia wito wa Serikali kwa kukubali kusaini mkataba wa kufadhili Mfuko wa Afya wa Pamoja. Hadi sasa wadau hao wamefikia tisa (9) ambao ni Benki ya Dunia (WB), Ireland, Uswisi, Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNPFA), Shirika la Kimataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), KOICA – Korea Kusini, Canada, Denmark na hatimaye Uingereza, baada ya kusainiwa kwa mkataba huu wa nyongeza. Siku ya leo ni sherehe kwetu baada ya kupata nyongeza ya mkataba,” amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuahidi kutoa fedha hizo ambazo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuahidi kuzipeleka fedha hizo kwa watakelezaji kwa wakati hususan kwa fedha zinazokwenda katika Vituo vya kutolea huduma za afya.