TANZANIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA AFYA
Posted on: October 5th, 2026Na Happyness Hans, WAF – Arusha
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za afya zinazovuka mipaka ya nchi, ikiwemo milipuko ya magonjwa, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza leo Oktoba 5, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Maryam Hemed kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, wakati wa Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) la Mawaziri Wanaohusika na Afya unaofanyika jijini Arusha , amesema changamoto hizo zinahitaji hatua za pamoja kutoka kwa nchi wanachama ili kuimarisha usalama wa afya katika ukanda huo.
Dkt. Hemed amesema Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na utoaji wa tahadhari za mapema, uwezo wa maabara, Timu za Mwitikio wa Haraka, usimamizi wa wagonjwa, kinga na udhibiti wa maambukizi, pamoja na mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii.
Amesema Ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya homa za virusi zinazosababisha kutokwa damu yanaendelea kuhitaji maandalizi endelevu ya kikanda, akieleza kuwa uzoefu wa milipuko iliyowahi kutokea katika ukanda huo umeonesha umuhimu wa utambuzi wa mapema, mwitikio wa haraka, uratibu madhubuti na ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti kuenea kwa magonjwa.
Aidha, Dkt. Hemed amesema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinapaswa kuendelea kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na saratani, kwa kuimarisha hatua za kinga, uchunguzi na ugunduzi wa mapema, pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma bora, dawa muhimu na teknolojia za afya.
Amesema ushirikiano wa kikanda pia unahitajika katika kuimarisha udhibiti na uhakiki wa ubora wa dawa, mifumo ya ununuzi na ugavi wa bidhaa za afya, utafiti, pamoja na kubadilishana maarifa na uzoefu ili kujenga mifumo ya afya iliyo imara na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya.