Wizara Ya Afya

SIMIYU KUTUMIA TATHMINI YA 'STAR RATING ASSESSMENT' KUBORESHA UTOAJI HUDUMA ZA AFYA

Posted on: October 27th, 2026

Na Zakayo Mosha WAF -SIMIYU

Mkoa wa Simiyu umejipanga kutumia vema matokeo ya zoezi la tathmini ya kuvipatia kategoria ya nyota vituo (star rating assessment) linaloendeshwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, katika Vituo vya kutolea huduma za afya ya Msingi ikiwemo Zahanati, Vituo vya Afya na katika Hospitali zote za Halmashauri Mkoani Simiyu.

Kauli hiyo imetolewa oktoba 27, 2026 mkoani Simiyu na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt.Yudas Ndungile wakati wa zoezi la tathmini ya kuvipatia kategoria ya nyota vituo vya kutolea huduma za afya kulingana na Ubora wa huduma zinazotolewa ( star rating assessment of all Primary Healthcare Facilities).

Amesema Mkoa wa Simiyu, umeendelea kupokea fedha nyingi kila mwaka kutoka Serikalini za ujenzi mpya na uboreshaji wa miundombinu, ununuzi wa madawa na Vifaa Tiba na ajira kwa wataalam wa afya, amesema kwa sasa hali ya upatikanaji wa Dawa katika Mkoa wa Simiyu ni zaidi ya asilimia 95.

"Zoezi hili la tathmini limeanza Mkoani hapa Oktoba 22, 2026 na litakapokamilika litasaidia kutoa picha halisi ya namna Vituo vyetu, Zahanati na Hospitali za Halmashauri namna gani vipo tayari na utoaji huduma bora za afya kwa Wananchi, hususani wakati huu wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote ngazi ya Msingi," amesema Dkt.Ndungile.

Aidha, amesisitiza kuwa,Mkoa wa Simiyu umejiandaa kukabiliana na athari zitakazojitokeza wakati wa mvua za El niño,ikiwemo Magonjwa ya mlipuko,amewaomba Wananchi kuendelea kuzingatia ushauri na maelekezo mbalimbali ya tahadhari yanayotolewa na Wizara ya Afya.

Dkt. Ndungile ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita Chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mfano bora katika kulinda Afya za Wananchi wake, amewataka Wataalam wa Afya mkoa wa Simiyu kufanya kazi kwa uzalendo,utu na moyo wa kuwahudumia Wananchi kwa upendo na huruma.