SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA LISHE KUPUNGUZA MADHARA YA UTAPIAMLO
Posted on: October 15th, 2026Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kinga, utambuzi wa mapema na matibabu ya utapiamlo katika vituo vya kutolea huduma za afya na ngazi ya jamii, kwa lengo la kupunguza madhara ya utapiamlo na vifo vinavyoweza kuzuilika, hususan kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, wakati wa majadiliano kuhusu mpango na mkakati wa kuimarisha lishe nchini katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, yaliyofanyika leo Oktoba 15, 2026.
Prof. Sunguya amesema utambuzi wa mapema na utoaji wa matibabu stahiki kwa watoto wenye utapiamlo ni muhimu katika kuzuia madhara yanayoweza kuathiri ukuaji wa mwili, maendeleo ya akili na afya zao kwa ujumla.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mwongozo wa Kitaifa wa Mwaka 2025 wa Kuzuia na Kudhibiti Ukondefu na Uvimbe Utokanao na Lishe kwa Watoto walio chini ya Miaka Mitano, ambao umesambazwa katika mikoa yote 26 ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa watoto wenye matatizo hayo.
Katika kuimarisha uwezo wa watoa huduma, Prof. Sunguya amesema wataalamu 267 wamejengewa uwezo katika awamu ya kwanza katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Lindi na Simiyu. Ameongeza kuwa Wizara inaendelea kupanua mafunzo hayo na kuboresha upatikanaji wa bidhaa zinazohitajika kwa matibabu ya utapiamlo.
Aidha, amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau imenunua katoni 2,585 za mchanganyiko wa vitamini na madini kwa ajili ya kuandaa chakula tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na boksi 2,150 za chakula tiba kilicho tayari kutumika kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo mkali.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kinga ikiwemo utoaji wa matone ya vitamini A kupitia Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto unaofanyika Juni na Desemba kila mwaka. Hadi Juni 2026, jumla ya watoto 8,738,461 walikuwa wamepatiwa vitamini A, sawa na asilimia 92 ya walengwa.