SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MIKAKATI YA KUDHIBITI MATUMIZI YA POMBE, SIGARA NA SHISHA
Posted on: October 19th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Dodom
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya kudhibiti matumizi ya pombe, sigara, shisha na sigara za kielektroniki, hususan miongoni mwa watoto na vijana walio chini ya umri wa miaka 18, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na jamii kwa ujumla.
Dkt. Magembe amesema hayo leo Oktoba 19, 2026, wakati akijibu hoja za Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, baada ya kuwasilishwa kwa taarifa kuhusu hali ya afya ya akili nchini, athari zake na mikakati ya Serikali ya kukabiliana na changamoto hizo.
"Udhibiti wa bidhaa hizi unahitaji ushirikiano wa Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, kwa kuwa masuala ya utoaji wa leseni za biashara, uzalishaji na usambazaji yanahusisha mamlaka tofauti, hivyo ni muhimu kuwa na mkakati wa pamoja unaolenga kulinda afya ya wananchi," amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali imeona umuhimu wa kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya akili na kupanua huduma hizo kuanzia ngazi ya hospitali hadi ngazi ya jamii ili kuwezesha wananchi kupata huduma mapema na kupunguza madhara yanayotokana na changamoto za afya ya akili.
Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za afya ya akili kwa wazee, akieleza kuwa kundi hilo linahitaji uangalizi na huduma zinazozingatia mahitaji yao huku jamii ikielimishwa ili kuepusha unyanyapaa dhidi ya watu wenye changamoto za afya ya akili.
Vilevile, ameeleza umuhimu wa kuimarisha Taasisi ya Afya ya Akili ya Mirembe ili iweze kuwa kituo cha kitaifa kinachochangia utoaji wa matibabu, mafunzo ya wataalamu, tafiti na usambazaji wa mbinu bora za huduma za afya ya akili nchini.
Dkt. Magembe amesema kuimarisha kinga, elimu kwa jamii, upatikanaji wa wataalamu na ushirikiano wa sekta mbalimbali ni miongoni mwa hatua muhimu za kukabiliana na changamoto za afya ya akili na kuboresha ustawi wa wananchi.