Wizara Ya Afya

SERIKALI KUPANUA USHIRIKIANO KATIKA UZALISHAJI WA DAWA ZA KIBAIOLOJIA

Posted on: October 27th, 2026

Na Clement Robert, WAF-Arusha

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema Tanzania inahitaji kujenga uwezo wa kuzalisha dawa za kibayolojia, ikiwamo insulini, chanjo na dawa nyingine maalumu, kwa kuwekeza katika teknolojia, wataalamu na miundombinu ya uzalishaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 27 wa Mwaka na Kongamano la Kisayansi la TAPHATA jijini Arusha Oktoba 27, 2026, amesema dawa hizo zina nafasi muhimu katika matibabu ya magonjwa mbalimbali, lakini baadhi yake zina gharama kubwa.

“Hapa ndipo Tanzania inapaswa kuingia, si kama mnunuzi wa mwisho, bali kama mzalishaji,” amesema Waziri Mchengerwa, akieleza umuhimu wa kujenga uwezo wa ndani katika uzalishaji wa dawa.

Amesema Tanzania inaweza kuanza kwa kuimarisha uzalishaji wa dawa za kemikali na malighafi zake, kisha kushirikiana na kampuni za kimataifa katika hatua za mwisho za uzalishaji kabla ya kujenga uwezo wa kuzalisha dawa za kibayolojia zinazofanana na dawa asilia, zinazojulikana kama biosimilars.

Amesisitiza kuwa hatua hizo zinahitaji ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, vyuo vikuu, viwanda vya dawa na mamlaka za udhibiti ili kuhakikisha uzalishaji unazingatia viwango vya ubora na usalama.

Aidha, amezitaka taasisi za elimu kuandaa wataalamu wenye ujuzi katika teknolojia ya kibayolojia, uhakiki wa bidhaa za kibayolojia na usajili wa dawa ili kukidhi mahitaji ya sekta hiyo.

Amesema Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), vyuo vikuu na viwanda vinapaswa kushirikiana katika utafiti na majaribio ya kliniki kwa kuzingatia sheria na maadili ya utafiti, ili kujenga msingi wa uzalishaji na ubunifu wa dawa nchini.