NHIF YATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: September 4th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Arusha
Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, amewataka watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuongeza kasi, ubunifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya bila kukumbana na vikwazo vikubwa vya kifedha.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Septemba 04, 2026, wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa katika ufungaji wa Mkutano wa Nne wa Baraza la Nne la Wafanyakazi wa NHIF uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jijini Arusha.
Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni agenda muhimu ya Taifa inayohitaji ushirikiano wa Serikali, NHIF, watoa huduma za afya, wananchi, waajiri, sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali, huku akisisitiza kuwa watumishi wa Mfuko wana nafasi kubwa katika kufanikisha azma hiyo.
“Tusisubiri wananchi waje ofisini kwetu, sisi twende kwa wananchi,” amesema Dkt. Samizi, akihimiza matumizi ya teknolojia, mifumo ya kidijitali pamoja na kampeni za uhamasishaji na elimu kwa umma ili wananchi wengi zaidi waelewe umuhimu wa kuwa na bima ya afya.
Aidha, Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na uadilifu katika matumizi ya rasilimali za Mfuko, akiwataka watumishi kutambua kuwa kila shilingi inayosimamiwa na NHIF ina dhamana kwa wananchi na hivyo kutumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Ameitaka Menejimenti ya NHIF kuendelea kuimarisha mifumo ya kupima utendaji wa watumishi na vitengo mbalimbali, sambamba na kupambana na vitendo vya rushwa, udanganyifu, ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za Mfuko.
Kuhusu utoaji wa huduma, Naibu Waziri amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kumweka mwananchi mbele, kwa kuhakikisha wanachama wanapokelewa kwa heshima, wanapata taarifa sahihi na huduma kwa wakati pamoja na kushughulikiwa kwa haraka kwa changamoto na malalamiko