Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MSITUMIE NYARA ZA SERIKALI KWENYE TIBA ASILI

Posted on: August 31st, 2024

Na WAF, Mwanza


Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ametoa wito kwa wataalamu wa tiba asili nchini kuachana na matumizi ya Nyara za Serikali kama ngozi za wanyama katika shughuli zao za kitabibu na badala yake wazingatie matumizi sahihi ya dawa zao. 


Dkt. Mollel ametoa wito huo leo Agosti 31, 2024 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrila yalio fanyika Kitaifa jijini Mwanza na ratibiwa na Wizara ya afya chini ya baraza la tiba asili na tiba mbadala.


“Tunahitaji kuondokana na imani hizi potofu ili kunusuru maisha ya wanyama pamoja na binadamu. Hakuna sababu ya kuendeleza matumizi haya ya viungo vya wanyama kwa kuwa ni hatari kwa mazingira na ustawi wa binadamu, Sisi sote tunapaswa kukemea vitendo hivi, kulinda mazingira, na kuhakikisha tunafichua wenye vitendo viovu”. Amesema Dkt. Mollel


Aidha, Dkt. Mollel ameitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya tafiti za kina kwa wataalamu wa tiba asili ya Mwafrika kwani NIMR inapaswa kufanya tafiti za kina kuhusu vyanzo vya dawa zinazotumika na kuhakikisha kuwa zinatunzwa vizuri na kuendelezwa kuzalishwa kwa wingi kwenye huduma zao.


Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu, Dkt. Ahmad Makuwani, amekiri kuwa dawa zinazozalishwa na wataalamu wa tiba asili zimefanya maendeleo makubwa, huku mataifa mengine kama Angola yakizisajili kama dawa rasmi kwa matumizi ya binadamu.


Kilele cha maadhimisho haya kimewakutanisha waganga wa jadi na wataalamu wa tiba asili, huku kikiwa na lengo la kuboresha huduma za tiba asili na kutetea haki za wanyama katika utendaji wa tiba hizi.