MIKOA KANDA YA ZIWA YASISITIZWA USHIRIKIANO KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA YA MAMA NA MTOTO
Posted on: September 26th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF – Shinyanga
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji katika Hospitali ya Bugando, Dkt. Samson Kitiba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa , amesema mafanikio katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto yanahitaji ushirikiano wa watumishi wote wa sekta ya afya kutekeleza wajibu kwa ufanisi katika eneo la kazi ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Dkt. Kitiba ameyasema hayo leo Septemba 25, 2026, mkoani Shinyanga, wakati akifunga kikao kazi cha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa Mikoa inayojumuisha Kanda ya Ziwa, ambapo amesisitiza umuhimu wa wataalamu kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kutumia ujuzi walioupata kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.
Amesema kikao hicho kimeonesha kuwa maeneo mbalimbali yana uzoefu na changamoto tofauti, hivyo ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalamu ni muhimu katika kupata suluhisho na kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
“Tunaposhirikiana kwa umoja wetu, tunaweza kuleta mabadiliko na kuokoa maisha ya mama na mtoto. Mabadiliko hayawezi kuanza kwa kusubiri mtu mwingine atubadilishe, bali yanaanza na sisi wenyewe,” amesema Dkt. Kitiba.
Aidha, Dkt. Kitiba amewataka watumishi wa afya kuachana na utendaji wa mazoea na kuwa wabunifu, wawajibikaji na wenye kutafuta suluhisho la changamoto zilizopo katika maeneo yao ya kazi, akisisitiza kuwa kuendelea kufanya mambo kwa mtindo wa mazoea hakutasaidia kuboresha huduma za afya.
Amesema pamoja na Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa tiba, ni muhimu watumishi kuzingatia utu, upendo, huruma na kutoa huduma inayomheshimu mteja, kwa kuwa ubora wa miundombinu na vifaa tiba pekee hauwezi kutosha iwapo wananchi hawapati huduma yenye heshima na kujali utu.
“Tunapomhudumia mama na mtoto, tunapaswa kuelewa kwamba tunashughulika na maisha ya mtu na mustakabali wa familia nzima. Huduma tunayotoa inaweza kuathiri maisha yao kwa muda mrefu, hivyo tunapaswa kuwahudumia kwa utu, upendo na huruma,” amesema.