MHE. MCHENGERWA AKABIDHI AMBULANCE, ATOA MAELEKEZO MAZITO KWA MADAKTARI NA WAUGUZI
Posted on: October 4th, 2026Na John Mapepele, WAF - DSM
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amekabidhi gari la wagonjwa (ambulance) lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 100 katika Kituo cha Afya Mpiji Magohe, Wilaya ya Ubungo, kwa lengo la kuboresha huduma za afya na kurahisisha usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo 3 Oktoba 2026, ambapo gari hilo linatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi wa eneo hilo
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mchengerwa amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mhe. Angela Kairuki, kwa juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuleta na kusimamia maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi katika kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo afya, huku akieleza kuwa uwepo wa ambulance hiyo utasaidia kurahisisha huduma za dharura kwa wagonjwa na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kuwahamisha kutoka kituo kimoja cha afya kwenda kingine.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amemwelekeza Katibu wa Wizara hiyo Grace Magembe kutoa waraka kwa wataalam wote wa afya kwenye hospitali zote nchini kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kuepuka kuomba rushwa.
"Haya ni maelekezo yangu nchi nzima kwa watumishi wa afya kwenye hospitali zote kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi hususan kwa mama na watoto wachanga kama maelekezo ya Mheshimiwa Rais" Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.
Amewaagiza Waganga Wakuu, wauguzi na wataalamu wa afya kuhakikisha wajawazito wanapokelewa na kuhudumiwa kwa heshima, utu na weledi wanapofika katika vituo vya afya.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupata huduma bora bila kufanyiwa vitendo vya kuwakejeli, kuwadhalilisha au kuwavunja moyo wakati wa kutafuta huduma za afya.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mhe. Angela Kairuki, amemshukuru mhe Waziri Mchengerwa na amesisitiza umuhimu wa kulitumia gari hilo kwa madhumuni yaliyokusudiwa.