Wizara Ya Afya

MCHENGERWA: TUJENGE MIRADI YA AFYA KWA UBORA KWA MANUFAA YA VIZAZI VYA SASA NA VIJAVYO

Posted on: October 4th, 2026

Na Clement Robert, WAF - Pwani, Rufiji

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka viongozi na watendaji wanaosimamia miradi ya afya kuhakikisha wanatumia ubunifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iwe na ubora na iweze kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Ameyasema hayo leo Oktoba 04, 2026, mkoani Pwani, wilaya ya Rufiji wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya cha Samia Suluhu Hassan.

Mchengerwa amesema Serikali inahitaji kuona miradi ya afya inayojengwa kwa fedha za umma ikitekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, huku akisisitiza umuhimu wa kuzuia ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za wananchi.

Amesema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, mabweni na Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan ni miradi yenye umuhimu mkubwa kwa wananchi, hivyo wahusika wanapaswa kuhakikisha inakamilika kwa ubora na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Nawaomba viongozi na watendaji wote tulinde fedha za umma na kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kutekeleza miradi hii, ili iweze kubeba na kufungua fursa zaidi kwa Watanzania,” amesema Mchengerwa.

Aidha, Mchengerwa amewataka viongozi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na uadilifu, akieleza kuwa mafanikio ya miradi ya maendeleo yanahitaji ushirikiano wa viongozi, wataalamu, wananchi na wadau mbalimbali.

Katika hatua nyingine, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuboresha miundombinu na huduma za afya nchini.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuelekeza fedha katika miradi ya afya katika mikoa, wilaya na halmashauri mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Mchengerwa amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye ufanisi katika maeneo yao.