Wizara Ya Afya

MCHENGERWA ATOA MAELEKEZO KWA KATIBU MKUU KUWEZESHA HUDUMA ZA KIBINGWA RUFIJI

Posted on: October 4th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF Pwani, Rufiji

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya pamoja na taasisi za afya kuhakikisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani inajengewa uwezo wa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa, ikiwemo huduma za figo, saratani na moyo.

Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 4,2026 Rufiji Mkoani Pwani wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani na Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo unapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya wataalamu na uwekaji wa vifaa tiba vinavyohitajika.

Aidha amemtaka Katibu Mkuu kuhakikisha huduma za magonjwa ya figo, ikiwemo huduma za kusafisha damu, zinapatikana katika hospitali hiyo ili wananchi wasilazimike kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Aidha, ameitaja Taasisi ya Saratani Ocean Road kuwa miongoni mwa taasisi zinazopaswa kushirikishwa katika maandalizi ya huduma za saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa vifaa na utaalamu unaohitajika.

Mchengerwa pia amemsisitiza Katibu Mkuu kuweka mazingira ya upatikanaji wa huduma za magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo, ili wananchi wa Mkoa wa Pwani na maeneo jirani waweze kupata huduma hizo karibu na maeneo yao.

“Tunataka huduma hizi zipatikane hapa hapa. Wananchi wasilazimike kwenda mbali kutafuta huduma za figo, saratani na moyo wakati tunaweza kuziweka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wetu,” amesema Mchengerwa.

Amezitaka taasisi hizo kufanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Afya katika kipindi cha ujenzi, ili maandalizi ya wataalamu, vifaa tiba na mifumo ya huduma yaanze mapema na kuhakikisha hospitali inaanza kutoa huduma zenye kiwango cha juu kwa wananchi mara itakapokamilika.