Wizara Ya Afya

MCHENGERWA AKEMEA WATENDAJI MOSHI NA MWANGA, AWATAKA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO

Posted on: July 25th, 2026

Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa amewataka Watendaji wa Serikali kusimamia vema utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuweka pembeni tofauti zao ili kuwaletea wananchi maendeleo

Kauli hiyo ameitoa leo wakati alipofanya kikao na viongozi wa Serikali na Siasa wa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake kama msimamizi wa Serikali wa mkoa huo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye mkoa huo.

"Itakuwa vigumu kutekeleza kwa ufanisi miradi mbalimbali maendeleo kama Watendaji wa Serikali wataendekeza kugombana badala ya kushirikiana". Amefafanua Mhe. Mchengerwa

Ameonya tabia hizo huku akisisitiza kuwa kuteuliwa kushika nafasi hizo haimaanishi kuwa hakuna watu wengine wenye uwezo wa kufanya kazi hizo bali bahati ya kuaminiwa na Mamlaka ya uteuzi hivyo hawana budi kuzitendea haki.

Akikagua mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi cha mjini moshi kinachojengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 18 chenye uwezo wa kuchukua zaidi ya magari 200 na abiria zaidi ya 600 kwa wakati mmoja amesisitiza kutunza miundombinu mara baada ya kukamilika na kuangalia jinsi kurejesha gharama hiyo.

"Mradi huu umetumia gharama kubwa ni vema tujipange kuangalia namna bora ya kurejesha gharama hii." Amefafanua Mhe. Mchengerwa

Aidha, ameutaka uongozi wa mkoa kuwa na jicho la karibu mara baada ya kukamilika mradi huo ili kusiwe na upendeleo wa upangishaji wa utoaji wa huduma katika kituo hicho.

Akikagua mradi wa ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo wa majengo mjini Moshi, Mhe. Mchengerwa amepongeza juhudi za Halmashauri ya Moshi kwa mradi huo ambapo amesema utasaidia kuwapa burudani wananchi hususan kwenye soka kwa kuwa wataweza kushuhudia timu kubwa za ligi ya daraja la kwanza tofauti na sasa ambapo wanalazimika kusafiri kwenda katika mikoa mingine.

"Niwapongeze kwa mradi huu kwani michezo ni "soft power" kwa taifa lolote. Naamini uwanja huu ukikamilika wananchi wa moshi na Kilimanjaro watazishudia Simba na Yanga hapahapa". Aliongeza Waziri Mchengerwa