MAFUNZO YA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO YAONGEZA UWEZO WA WATAALAMU WA AFYA WILAYA YA SONGWE
Posted on: July 14th, 2026Na Happyness Hans, WAF- Songwe
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Songwe, Dkt. Benjamin Switi, amesema wataalamu wa afya wa hospitali hiyo wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa na wataalam kutoka Wizara ya Afya yenye lengo la kuwaimarisha katika kujikinga dhidi ya maambukizi wanapotoa huduma kwa wagonjwa, hususan wakati wa milipuko ya magonjwa.
Amesema hayo leo Julai 14, 2026 mkoani Songwe, Dkt. Switi amesema mafunzo hayo yamejikita katika kuimarisha uelewa kuhusu ugonjwa wa Ebola, ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga, uvaaji na uvuaji wa mavazi maalumu, pamoja na kuzingatia kanuni za kudhibiti maambukizi wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa au wahisiwa wa ugonjwa huo.
Aidha, Dkt. Switi amesema kuwa ujuzi walioupata utaongeza utayari wa hospitali kukabiliana na milipuko unaoweza kujitokeza, huku ukiwawezesha wataalamu kutoa huduma salama na zenye kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Frederick Myula, amesema timu hiyo ipo mkoani Songwe kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika utoaji wa huduma za dharura na mahututi, sambamba na kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
Dkt. Myula amesema washiriki wamepatiwa mafunzo ya namna sahihi ya kuvaa na kuvua mavazi ya kujikinga pamoja na mbinu salama za kumhudumia mgonjwa au mhisiwa wa Ebola.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora, salama na zenye ubora katika kila ngazi ya utoaji huduma.
Naye Afisa Muuguzi wa Idara ya Dharura, Ajali na Mahututi katika Hospitali ya Wilaya ya Songwe, Agustino Madoshi, amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa wa kina kuhusu namna ya kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan Ebola, pamoja na matumizi sahihi ya mavazi maalumu ya kujikinga wakati wa kumhudumia mgonjwa.