HUDUMA ZA AFYA ZA KINGA ZAENDELEA KUIMARIKA MKOA WA PWANI
Posted on: June 19th, 2025
WAF Pwani
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma za afya za kinga na huduma za afya ngazi ya jamii nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii.
Hayo yamebainishwa Juni19, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Otilia Gowelle, alipofanya ziara ya kikazi mkoani Pwani ili kufuatilia na kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya na maendeleo ya mafunzo kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) katika mkoa huo.
Akiwa katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha, kinachotoa mafunzo kwa CHWs, Dkt. Gowelle amewatia moyo na kuwataka kuzingatia masomo yao kwa bidii ili kutoa huduma bora na zenye kuzingatia maadili na viwango vya taaluma.
“Nawasihi msome kwa juhudi na maarifa ili mkitoka hapa muwe tayari kutoa huduma zenye ubora, kuisaidia jamii kukabiliana na changamoto za kiafya na kuchangia katika kufikia lengo la afya kwa wote,” amesisitiza Dkt. Gowelle.
Sambamba na kutembelea chuo, Dkt. Gowelle alifika katika kata ya Misugusugu, Halmashauri ya Mji Kibaha, ambapo alikutana na CHWs walioko kazini na kushuhudia jinsi wanavyotekeleza majukumu yao chini ya usimamizi wa wataalam wa zahanati ya Misugusugu.
Alifurahishwa na namna wanavyoshirikiana kutoa huduma za kinga, tiba ya msingi, lishe na ustawi wa jamii.
Vilevile, CHWs walipata nafasi ya kueleza mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya vitendea kazi na masuala ya usafiri ndipo Dkt. Gowelle akaahidi kuwa Wizara itashirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa suluhu na mazingira ya kazi yanaboreshwa.
Katika ziara hiyo Dkt. Gowelle iliambatana na Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii, Dkt. Norman Jonas Kyala.
Ziara hiyo ni muendelezo wa juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii kwa kuhakikisha utoaji wa huduma bora unaenda sambamba na mafunzo na usimamizi endelevu katika ngazi zote za utekelezaji.