Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI AWATAKA WANAWAKE KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA SARATANI

Posted on: September 5th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka wanawake nchini kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya, hususan vipimo vya saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti, angalau mara moja kila mwaka wa kuzaliwa ili kuwezesha kubaini dalili za magonjwa hayo mapema na kupata matibabu kwa wakati.

Dkt. Samizi ametoa wito huo leo Septemba 06, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa nembo ya Taasisi ya Mariam Mungula Foundation, taasisi inayolenga kuisaidia jamii, hususan wanawake, kupitia utoaji wa elimu na uhamasishaji kuhusu afya na masuala mbalimbali ya uzazi, ikiwemo changamoto zinazohusiana na ukomo wa hedhi.

Amesema uchunguzi wa mara kwa mara ni hatua muhimu katika kujilinda dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na saratani, akisisitiza kuwa kubaini ugonjwa katika hatua za awali huongeza fursa ya mgonjwa kupata matibabu kwa ufanisi zaidi.

Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika vifaa, teknolojia na huduma za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa saratani, ikiwemo saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.

Amesema uwekezaji huo unaenda sambamba na juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wakati, huku akiwataka wanawake kutumia fursa zinazopatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao.

Aidha, Naibu Waziri amelitaka Taasisi ya Mariam Mungula Foundation kutumia nafasi yake kuendelea kutoa elimu sahihi kwa jamii, hususan wanawake, kuhusu umuhimu wa kujikinga na magonjwa, kufanya uchunguzi wa afya na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi binafsi, mashirika na jamii ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha juhudi za kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya, ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Samizi amesisitiza kuwa afya ni jukumu la kila mmoja, hivyo wanawake wanapaswa kuweka uchunguzi wa afya kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku ili kulinda afya zao na familia zao.