DKT. SAMIZI AWATAKA VYUO VYA AFYA KUJENGA MAADILI KWA WANAFUNZI
Posted on: September 16th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Kibondo
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka wakuu wa vyuo vya afya nchini kuhakikisha wanafunzi wanajengwa katika misingi ya maadili mema, weledi na uwajibikaji ili kuwaandaa wahudumu bora wa afya watakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma zenye ubora na kuisaidia jamii.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo, Septemba 16, 2026, wakati akitembelea vyuo vya afya vilivyopo Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma, kwa ajili ya kukagua hali ya utoaji wa huduma pamoja na miundombinu ya vyuo hivyo.
Amesema kuwa utoaji wa elimu ya kitaalamu pekee hautoshi, bali wanafunzi wanapaswa kujengewa maadili mema, nidhamu, huruma na uzalendo ili wanapohitimu wawe watumishi wanaoweza kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia taaluma na utu.
Katika ziara hiyo, Dkt. Samizi ametembelea eneo la ujenzi wa hosteli za Chuo cha Uuguzi na kumwelekeza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi.
Aidha, Dkt. Samizi ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Kibondo pamoja na Kituo cha Afya, ambapo amekagua hali ya utoaji wa huduma na kuwatembelea kina mama waliojifungua, huku akiwapatia zawadi kama sehemu ya kuwatia moyo na kuwapongeza kwa kujifungua salama.
Sambamba na hilo, amewakumbusha wananchi wa Wilaya ya Kibondo kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa bima hiyo ni miongoni mwa njia muhimu za kusaidia wananchi kumudu gharama za matibabu na kupata huduma za afya pale wanapozihitaji.
Dkt. Samizi amesisitiza wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika sekta ya afya na kuendelea kushirikiana na watoa huduma ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote.